EMBRACE –
Tushikamane:
Kupunguza
vifo kupitia uhamasishaji jamii na vikundi vya wanawake
Mradi wa Tushikamane unalenga ‘Kupunguza
vifo wakati wa ujauzito na utotoni’
Jina la Mradi kwa Kiingereza ni EMBRACE kifupisho
cha
‘ Empowering Mothers and Babies to Receive
Adequate Care & Equality’
Maana yake: Kuwawezesha Akinamama na Watoto
Wachanga kupata
Matunzo ya Kutosha, na Usawa
Kusudio la Mradi:
Kupitia uwezeshaji na elimu kwa wanawake,
Mradi unatarajia kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika, na kuleta ahueni
endelevu inayogusa nyanja mbalimbali za maisha ya watu wenye hali duni waishio
vijijini Tanzania.
Tatizo: Vifo
vya kushitikisha vya wanawake na watoto wachanga sehemu za vijijini Tanzania.
Mwaka 2013, kote duniani, jumla ya wanawake 289,000 walipoteza maisha kutokana na matatizo
yanayohusiana na ujauzito na kujifungua.
Kwa kila mwanamke mmoja anayepoteza maisha, takiriban wanawake wengine 20
hupatwa na majeraha makubwa, maambukizi au ulemavu.
Maeneo mengi ya Tanzania vijijini hukumbwa na matukio
mengi haya ya kusikitisha ambayo yangeweza kuepukika: Kila siku, wanawake 35 hufariki kutokana na
sababu zinazohusiana na kujifungua. Katika maeneo ya vijijini, mtoto 1 kati ya
watoto 10 hufariki kabla ya kutimiza miaka 5. Idadi isiyojulikana hupatwa na
madhara mengi mabaya kama vile kuharibika ubongo.
Katika maeneo ya vijijini
ambayo hayafikiki kwa urahisi kama vile Tunguli, kwa ukweli, karibia mwanamke 1 kati ya 100 hufariki wakati wa kujifungua. Sababu 5
kuu za vifo hivyo zinaweza kudhibitiwa: kupoteza damu nyingi, sumu kutokana na
maambukizi kuenea kwenye damu (sepsisi), mtoto kukwama kutoka, kifafa cha mimba,
na utoaji mimba kwa njia zisizo salama. Kila kifo cha mama ni pigo kubwa kwa kijiji chake kizima – nani
atawalea watoto wake wengine, na kuhangaika na majukumu mengine ya kimaisha ya
kila siku ?
Kuna sababu nyingi zinazoingiliana ambazo huchangia matatizo haya ya msingi kutoshughulikiwa ipasavyo,
kwa mfano: kutopata huduma za afya; ukosefu wa usawa kijamii; kukosa elimu; magonjwa
yasiyopona ; utapiamlo; mgonjwa kutakiwa kusafiri mbali kupata huduma; kutozingatia
uzazi wa mpango; na huduma duni za usafiri. Mzizi wa haya yote ni kwamba
asilimia 90 ya idadi ya watu wote huishi kwa kipato cha dola 2 (Shs 4,200/-) kwa siku au
chini yake.
Hospitali ya Berega huhudumia eneo kubwa
lisilofikika kwa urahisi Tanzania vijijini lenye watu takriban 217,000. Kuna
vizazi 8,500 kwa mwaka, ambapo watoto 1,000
tu ndio huzaliwa kwenye kituo cha afya. Kituo cha afya cha Tunguli huhudumia eneo lenye mraba karibia kilomita
625 na kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012,
eneo hii linaweza kujumuisha watu 20,000, (ingawa siyo wote hutumia ipasavyo huduma
za Kituo cha Afya cha Tunguli ).
Kwa nini
tuanze kwa kuihamasisha
jamii na vikundi vya wanawake ?
Kwa nini tusiende kwenye matatizo moja kwa moja ?!
Katika kushughulikia jambo lenye kuhitaji ufumbuzi
wa haraka, unaweza kushawishika kutoa ufumbuzi wa moja kwa moja –mathalan kujenga zahanati, kuanzisha
kiliniki ya uzazi wa mpango, kutengeneza miundombinu nk. Kutoa ufumbuzi wa moja
kwa moja ndiyo njia sahihi ya kufanya, ili mradi ufumbuzi huo uwashirikishe
wanajamii, na ili mradi kuwepo na shinikizo au msukumo wa muda mrefu wa
kuboresha hali husika. Hata hivyo, ukweli usiofurahisha ni kwamba kawaida Barani
Afrika, jitihada za ufumbuzi mara nyingi hufanyika bila kuwashirikisha wanajamii
ipasavyo, na mara nyingi hakuna makakati wa muda mrefu wa ufuatiliaji baada ya
hapo. Juhudi kama hizi mara nyingi husuasua, na kawaida hushindwa kupunguza
vifo: vifaatiba huharibika; mbinu bora mpya
za utendaji hazizingatiwi, watu
hushindwa kuhudhuria; na zana hukosa matunzo nk.
Hasa kuhusiana na ufumbuzi unaotokana na misaada ya wafadhili wa nje, kama jamii
hazioni miradi au huduma hizo kuwa zao,
basi zinakuwa hazijalenga vipaumbele kwa usahihi. Hakika, vigezo muhimu ambavyo huchochea vifo vya mama na watoto vimegemea kwenye tabia za wale ambao mara nyingi sauti zao hazisikiki vya kutosha katika maamuzi: wanawake – mathalan katika kutafuta huduma za uzazi wa mpango, huduma
za uzazi hospitalini, au chanjo; matumizi ya maji safi na salama na vyandarua; kuendelea
na unyonyeshaji; uelewa wa lishe bora
kwa watoto; kutambua magonjwa
hatari; nk. Katika kaya ambazo bado zimegubikwa sana na mfumo dume, wanaume wanaweza kutoelewa fika
vipaumbele muhimu katika kuokoa maisha
ya mama na watoto.
Kama kinachohitajika kubadilishwa ni tabia za
wanawake walio katika umri wa uzazi, ufumbuzi siyo wageni au wafadhili kutoka nje kuja na kuwambia nini cha kufanya. Njia sahihi
ni kuanza na kutoa elimu na kujenga uelewa, lakini kwa njia ambayo inatengeneza
wanawake mifano ndani ya jamii husika, ili wanawake wengine waweze kuiga kutoka kwao tabia na utendaji ambavyo vinaweza kuchangia kuepusha vifo. Wanawake
wanapaswa kuwa na sauti kubwa zaidi.
Sauti kubwa ya wanawake, baadae, itachangia utambuzi wa mahitaji mengi ya msingi kama vile usafiri, uzalishaji shambani,
ajira, maji, chakula, upatikanaji wa huduma za afya za msingi nk. Kushughulikia
mahitaji haya ya msingi, baada ya jamii kuyabaini kama mahitaji yao na kuyapa kipaumbele,
kutachangia miradi au huduma zitakazoanzishwa kufanikiwa.
Kutokana na
ushahidi katika nchi kadhaa, ni wazi kuwa njia bora ya kufanya kazi na wanawake
walio katika umri wa uzazi ni kupitia vikundi
vya wanawake kwenye jamii zao. Ingawa
vikundi huanza kwa kuwaleta pamoja wanawake wenye umri mdogo, hatimaye
huwaingiza wanawake wote ambao sauti zao zinapaswa kusikika, wakiwemo wanawake
wenye umri mkubwa zaidi, wanaume, na wale ambao wajibu wao unagusa afya ya mama
na mtoto. Kikundi kinachozaliwa hujulikana kama Kikundi
cha Kujifunza na Utendaji
Shirikishi (Participatory Learning &
Action Group)
Vikundi vya Kujifunza na Utendaji Shirikishi (Tushikamane Groups)
Vikundi vya Kujifunza na Utendaji Shirikishi au
Vikundi vya Tushikamane vitajaribu kupunguza vifo vya akinamama na watoto kwa kutoa nafasi
ya mijadala mahali ambapo wanajamii na hususan wanawake, hupewa fursa sawa
kuchangia na kutoa mawazo yao, na kuweza kubainisha vipaumbele miongoni mwa matatizo yote yanayosababisha vifo.
Njia
hii itaelekeza katika utambuzi wa mahitaji
ya jamii na ufumbuzi wake kutoka kwa jamii yenyewe, ufumbuzi ambao utazingatia
mambo mengi - zaidi ya afya; yakiwemo kushughulikia elimu, usafirishaji, maji, huduma ya vyoo na
usafi wa mazingira, chakula, agronomia (sayansi mseto ya kilimo bora cha mazao sambamba na utunzaji wa afya ya udongo), uzazi
wa mpango na umasikini( kama ambavyo miradi yenye mafanikio makubwa kama ile
inayoendeshwa na Shirika la Hands 4 Africa
tayari imeonesha!).
Mtandao
mpana wa kusaidiana wa Tushikamane, baada ya hapo, unaweza kuisaidia jamii
kubuni, kutekeleza na kutathmini njia za ufumbuzi zinazofaa
ambazo zimetokana na jamii yenyewe. Iwapo kila mmoja atafanya kadri ya
uwezo wake, lakini kwa kushirikiana na mtandao mzima, washirika, wakala wa
kujitolea, na juhudi mbalimbali ndani na nje, jamii ya Tunguli inaweza
kufanikisha juhudi zao za kutatua
matatizo yanayoikabili, wakitumia njia
au mbinu endelevu ambazo wamezichagua
baada ya kuzijadili kwa makini na kuzitekeleza vizuri. Kwa mfano kampeni ya kukuza unyonyeshaji wa maziwa ya
mama; chati za maendeleo ya mtoto; mifumo ya vyoo na usafi wa mazingira; huduma
ya chanjo ; visima vilivyofunikwa; huduma ya usafiri wakati wa dharura yenye
gharama nafuu; uzazi wa mpango; kilimo cha mazao ya chakula na biashara; kuzuia
malaria; kuzuia upungufu wa wekundu wa damu (anemia); mafunzo kwa wakunga wa
jadi; vikundi vya elimu ya wanawake; nk.
Vikundi vya Tushikamane huanza na wanawake wenye umri wa uzazi (16-49). Wajawazito, akinamama
vijana na wasichana katika umri wa balehe watapewa hamasa ya kipekee
kuhudhuria. Kadri muda unavyokwenda, wanajamii wote ambao wanaguswa na masuala
ya afya ya mama na watoto wachanga, wakiwemo wanaume, wanawake wenye umri
mkubwa zaidi na viongozi wa jamii wataweza kuruhusiwa kuhudhuria na
wataeleweshwa kwa nini vikundi hivi
vinawalenga hasa wanawake na watoto.
Vikundi
vya Tushikamane siyo vikundi vya elimu ya afya mahali ambapo mwezeshaji hutoa
ujumbe kwa wanakikundi kama mwalimu. Badala
yake, vikundi vya Tushikamane ni fursa ya majadiliano mahali ambapo wanawake na
wanajamii hutambua matatizo yao na kuweka vipaumbele, halafu hubuni na
kutekeleza njia za ufumbuzi zinazofaa ambazo zimetokana na jamii yenyewe.
Majadiliano
hufanyika kupitia vikao vya kikundi 14 ambavyo
vimewezeshwa vizuri, na katika kila kikao huwa kuna mada mahsusi, na lengo
mahsusi. Mikutano hiyo hufanyika kupitia awamu 4. Vikundi vitaongozwa kupitia awamu zote 4, na mzunguko wa kujifunza
na utendaji shirikishi(PLA), na Wawezeshaji - Ester Paul au Rehema
Semwali.
Kama
sehemu muhimu ya ufuatiliaji wa mchakato
huu wa kujifunza na utendaji shirikishi, Mradi wa Tushikamane pia utajaribu kutathmini matokeo
ya mradi, kubaini yapi muhimu ambayo tumejifunza kutokana na mradi kabla ya uwezekano wa
kuupanua mradi siku za usoni. Tathmini
hii itasaidiwa na zoezi lililofanyika
hivi karibuni la kuchora ramani na kukusanya
taarifa za eneo la mradi, pamoja na kurasimisha majina
ya vijiji na vitongoji.
MAELEZO YA JUMLA JUU YA MZUNGUKO WA
UTENDAJI WA KIKUNDI CHA
TUSHIKAMANE
Vikundi vya TUSHIKAMANE vitaoongozwa na
Wawezeshaji kupitia mzunguko wa kujifunza na utendaji shirikishi (participatory
learning and action cycle) wenye awamu 4 na jumla ya mikutano 14 .
Mchakato
huu wa kikundi cha Tushikamane huchukua muda gani?
Mchakato wa kuunda kikundi na kuwa timu unaweza kuchukua takriban miezi 2. Vikundi vinaweza kukutana takriban kila baada
ya wiki 2, na siyo chini ya kila mwezi, kutegemea na utaratibu unaokubalika
zaidi kwao. Utekelezaji wa mikakati itakayokuwa imebainishwa unaweza kuchukua
kati ya miezi 2 hadi 6. Hivyo, unaweza kutarajia ratiba ifuatayo kwa ajili ya
utekelezaji wa mpango huu wa Tushikamane:
Uundaaji
kikundi na kujenga timu
|
Miezi
2 – 4
|
|
Awamu1:
Utambuzi wa pamoja wa matatizo
|
Mikutano
5
|
Miezi
2.5 – 5
|
Awamu
2: Utambuzi wa pamoja wa njia za
ufumbuzi
|
Mikutano
3
|
Miezi
1.5 – 3
|
Awamu
3: Utekelezaji wa pamoja wa njia za
ufumbuzi
|
Mikutano
3
|
Miezi
1.5 – 3
|
Utekelezaji wa njia za ufumbuzi
|
Miezi
3 – 6
|
|
Awamu
4: Kufanya tathmini pamoja
|
Mikutano
3
|
Miezi
1.5 – 3
|
Jumla
|
Miezi 12 – 24
|
Hadi hapo tumesema nini?
Maelezo ya jumla ya mradi wa Tushikamane:
Tutazishirikisha jamii kwa ukamilifu.
Tutazishirikisha kwa kuunda Kikundi katika kila kitongoji.
Sehemu zingine, kila kikundi kimeitwa ‘Kikundi cha Kujifunza na Utendaji Shirikishi kwa ajili ya Afya ya Mama na Mtoto’. Katika
Mradi wa Tunguli, kitaitwa Kikundi cha TUSHIKAMANE( Mkutano wa Kufanya kazi
Pamoja au Mkusanyiko wa Uwezeshaji). Kila kikundi kitapitia mzunguko wa
mikutano 14 ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kuiwezesha jamii kuamua shughuli gani muhimu zitapewa kipaumbele
katika kupunguza vifo vya akinamama na watoto wachanga
Kuanzisha Vikundi vya Tushikamane
– kujitayarisha kuanza
Kuwashawishi wanajamii
wanaostahili kuhudhuria
Watu
ambao wanaathiriwa zaidi na tatizo
wanapaswa kushirikishwa katika uchambuzi wa hali inayowaathiri na kufanya uamuzi wa nini kifanyike. Kwa hivyo, RS na EP watahamasisha wanawake walio katika umri wa
uzazi kuhakikisha wanajiunga na vikundi
hivi. Wanawake hao wenyewe ndiyo watakaoamua juu ya uanachama katika kikundi.
RS na
EP watawahimiza kutoa kipaumbele kwa wajawazito na mama wenye umri mdogo,
pamoja na wanawake walioolewa na wasichana balehe, hasa akinamama na wasichana balehe kutoka katika kaya zenye hali duni
zaidi.
Tutawataka
waruhusu mwanajamii yoyote yule ambaye
anaguswa na vifo vya akinamama na watoto.
Tunataka hatimaye wanachama wa kikundi wajumuishe wale wote wanaowahudumia
akinamama na watoto kupitia ujauzito,
kujifungua na baada ya kujifungua. Hii inaweza kujumuisha, mathalan, wakunga
wasaidizi; wafanyakazi wa afya vijijini; viongozi wa jamii wa eneo husika;
wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali au wafanyakazi wa ugani au kwenye
miradi ya serikali katika eneo hilo; nk
Ester & Rehema watawashawishi wote kuhudhuria vikundi hivi ambavyo
vinaanzishwa.Watahakikisha
kuwa wanakikundi wote wnatambua kuwa wajibu wao katika kikundi utakuwa ni
kusikiliza na kuheshimu maoni na mawazo ya wanakikundi wakike, halafu kutoa
ushauri na msaada pale panapostahili ili kufanikisha lengo la kuboresha afya ya
mama na watoto.
Mwenyekiti
wa Kikundi na Kamati
Kila
kikundi kinaweza kuamua kuchagua kamati na,
au kutoa majukumu mahsusi kwa baadhi ya
wanakikundi. Kamati ijumuishe hasa wanawake-robo tu ndiyo wawe wanaume. Kamati
zichague mwenyekiti, na katibu mwanzoni kabisa.
Mwenyekiti
anapaswa kuwa mwanamke. Wajibu wa Mwenyekiti ni kukiongoza kikundi. Wajibu huu
unajumwisha kuongoza shughuli za kikundi na kutoa dira, kuwasimamia wanakamati
na wanakikundi na kukiwakilisha kikundi kwenye mikutano au shughuli
zinazostahili katika ngazi ya jamii, wilaya na kitaifa .
Wajibu
wa Katibu ni kuchukua na kutunza kumbukumbu za shughuli za kikundi. Hii
inajumuisha kujaza kitabu cha mahudhurio na kuandaa taarifa ya mkutano kila
baada ya mkutano kufanyika.
Kadri
kikundi kitakvyokua kinakua, kutahitajika kuwepo mweka hazina, wajibu wake
ukiwa ni kufuatilia fedha za kikundi na rasilimali zingine za kikundi.
Wajumbe
wa Kamati wote wana wajibu wa kuwashawishi wanajamii kujiunga na Kikundi , na
kushiriki katika mikutano. Wajumbe wa Kamati pia wana wajibu wa kuwasaidia Wawezeshaji (Rehema au Ester) wakati wa
mikutano.
Wanajamii wangapi wanatakiwa
kuandikishwa kwenye Kikundi?
Idadi
kuu ya wanakikundi waliosajiliwa inatakiwa kuwa takriban 50. Uanachama
ni wazi na hivyo inawezekana idadi kuu ya wanakikundi ikaongezeka katika uhai
wa kikundi.
Hata
hivyo, siyo wanakikundi wote waliosajiliwa wataweza kuhudhuria kila mkutano wa
kikundi. Kuhakikisha ushiriki wa kiwango cha juu, idadi ya wanakikundi
waliosajiliwa katika kila kikao inapaswa kuwa kati ya 25-30. Kukiwa
na zaidi ya idadi hii, inakuwa vigumu kwa kila mjumbe kushiriki na mwezeshaji
kumudu kikundi. Mikutano inastahili kuhudhuriwa angalau na wanakikundi 10 ili
iweze kuwa na tija. Kama idadi ndogo ya
hapo itahudhuria, mwezeshaji na wanakikundi waliopo wanaweza kuzunguka kwenye
kaya na kuwaleta washiriki wengine. Kama idadi ya wahudhuriaji ni ndogo sana, ni bora kuahirisha mkutano na
kuandaa kwa ajili ya tarehe nyingine.
Hali
halisi na takwimu kuhusiana na ukubwa wa vikundi katika maeneo ya vijijini
Tanzania
Ushahidi
unaonesha kuwa vikundi hufanikiwa zaidi pale angalau asilimia 30 wanakikundi
wanakuwa wajawazito. Kutokana na takwimu
za Sensa ya Tanzania, tuliweza kukokotoa na kufanya makadirio juu ya ukubwa wa
kikundi:
Takwimu hizi zinatoka: http://www.nbs.go.tz/nbs/takwimu/references/Tanzania_in_figures2012.pdf:
Nchini Tanzania kuna mfumo rasmi wa vijiji
na vitongoji. Kitongoji kina kaya 100. Kijiji kina vitongoji 3-4
. Kama kikundi kimoja kitahudumia mathalan watu 700 , basi katika
maeneo ya vijijini Tanzania hii ingemaanisha:
·
Kitongoji
kimoja kina watu takriban 700, ( watu 7 katika kila kaya);
·
hii
inafunika takriban eneo la kilomita 6 x
4, (kama kipimo cha idadi ya watu
kwa eneo ni watu 31 kwa kila eneo la mraba wa kilomita moja;
·
(ambapo angalau thelusi tatu ya akinamama
wanapaswa kuwemo katika kikundi);
·
Huenda
kukawa na wanawake walio katika umri wa uzazi 175 , (kwa sababu hujumuisha robo ya
idadi ya watu)
·
Wenye
afya ambao baadhi yao huendelea kupata watoto zaidi ya 6 (idadi ya watoto
kwa kila mwanamke 6.3)
·
Kwa
kiwango cha vifo vya akinamama cha
mwanamke 1 kwa kila wanwake 200 wanaojifungua kote nchini Tanzania , na
huenda kifo cha mwanamke 1 kwa kila 100-150 wanaojifunguakwenye maeneo ya
vijijini, kunakuwa na kifo 1 cha mwanamke kila miaka 5 katika kila kitongoji/au
kikundi cha wanawake;
·
Kila
kitongoji chenye watu 700 kinaweza
kupata vizazi 28 mwaka, (Makadirio ghafi ya vizazi 39);
·
Kati
ya hao, huenda watoto wachanga 2 chini
ya umri wa mwezi mmoja na mmoja zaidi chini ya miaka 5 watakufa kila
mwaka katika kila kitongoji.
Kukiwa na mwezeshaji mmoja akihuhudumia
vitongoji 3, atakuwa akihudumia takriban watu 2,000. Hii inaweza kumaanisha kuwa
kila mwezeshaji ataanza akiwa na
jukumu la kuepusha angalau kifo cha mama mmoja kila takriban
miaka 2, na karibia vifo vya watoto 7 kila
mwaka. Hii ni changamoto kubwa kwa mradi au afua yoyote ile.
Kuhakikisha makundi ambayo tayari yapo
kwenye jamii yanashirikishwa
RS na EP watahitaji kujua ni shughuli gani ambazo
mashirika mengine na jamii tayari zinatekeleza au zimepanga. Hii ni muhimu
kuhakikisha kwamba hakuna kurudia shughuli ambazo tayari zimeazishwa na pia kwamba mipango yote inasabihiana au kuimarisha
shughuli ambazo zinaendelea. Kama tayari
kuna vikundi kwenye jamii ambavyo vinatoa huduma, na ambavyo mnaweza
kushirikiana, basi vinapaswa kualikwa, wakati mwafaka, kutuma uwakilishi kwenye
kikundi cha Tushikamane kinachoanzishwa.
Ester na Rehena wanapaswa
kukutana na
·
Wenyeviti wa Vijiji;
·
Mashirika ya ngazi za wilaya, kama vile
mashirika yanayotoa misaada na mashirika
yasiyo ya kiserikali;
·
Maafisa wa serikali na juhudi zingine za
kiserikali;
·
wabia wengine wowote ili kupata taarifa juu ya
vikundi vingine vilivyopo.
Kikundi cha Tushikamane
kitakuwa na uhai wake wa pekee, lakini kinalazimika kufanya kazi kwa maelewano
na ushirikiano na juhudi na vikundi
vingine vilivyopo kwenye jamii.
Mara baada ya vikundi kuanzishwa
…
Mara
baada ya vikundi vya Tushikamane kuanzishwa kwa ukamilifu, vinahitaji kuanzisha mchakato
wa kujadili na kutambua masuala gani yanayosababisha vifo vya mama na watoto
wachanga ambayo yanapaswa kupewa
kipaumbele. Mijadala hii inapaswa kufanyika kupitia mfululizo wa mikutano 14 itakayoandaliwa na Rehena na Ester, chini ya uongozi na usimamizi wa Alex Gongwe; na kuwezeshwa na Wilbard Mrase na Mchungaji Isaac Mgego.
Mwishoni
wa mikutano 14, kutakuwa na tathmini rasmi ambayo itapima ufanisi wa mchakato
mzima.Kama mchakato umekwenda vizuri, mchakato mwingine wa mikutano 14 utaanza
tena kutafuta vipaumbele vipya. Kwa sababu hii mchakato huu hujulikana kama Mzunguko
wa Kujifunza na Utendaji Shirikishi (‘PLA
Group Cycle’).
MZUNGUKO WA UTENDAJI WA KIKUNDI CHA
TUSHIKAMANE
Awamu ya 1: kubaini matatizo
pamoja
Shabaha ya Awamu 1 ya mzunguko wa mikutano ni Kikundi kubainisha matatizo ya
afya ya mama na watoto wachanga ambayo yatapewa kipaumbele
Yafuatayo
ni maelezo ya jumla juu ya mikutano 14.
Maelezo yake kwa kirefu yatatolewa kwenye Kiongozi cha Mafunzo.
Mkutano wa 1: Kukiandaa kikundi
kuanza kazi
Malengo ya mkutano ni:
·
Kuutambulisha mpango katika mazingira ya jamii
husika
·
Kutambulisha utaratibu wa ‘kujifunza na utendaji
shirikishi’ (‘Participatory Learning and
Action’)
·
Kuunda kamati ya kikundi na kuweka sheria za
kuwaongoza wanakikundi
Mkutano wa 2: Kubaini matatizo ya afya
yanayowakumba akinamama
Lengo la mkutano ni :
·
Kujadili hali halisi ya matunzo ya nyumbani ya mama
waliojifungua na mienendo yao katika kutafuta huduma zinazostahili
·
Kubaini matatizo ya kiafya yanayowakumba wanawake
wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua
Mijadala katika mikutano ya vikundi itachochewa na Rehena
na Ester kwa kutumia zana maalum ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya lengo hilo– mathalan kadi za picha ambazo zinaonesha matatizo ya
akinamama na watoto wachanga chini ya wiki 4, mambo yanayochangia, na njia za
kuzuia au kudhibiti matatizo hayo ya kawaida.
Kuna jumla ya kadi 60 :
·
Kadi za matatizo(kadi 21): zinaonesha matatizo
makubwa ya kiafya ambayo yanawakabili
akinamama na watoto wachanga chini ya wiki 4
·
Kadi za mambo yanayochangia ( kadi 17): zinaonesha
mambo muhimu ambayo yanachangia matatizo hayo.
·
Kadi za shughuli za uzuiaji wa matatizo hayo (kadi
13 ): zinaonesha shughuli muhimu ambazo watu wanaweza kufanya ili kuzuia
matatizo yanayowakumba akinamama na watoto wachanga kutokea.
·
Kadi za shughuli za usimamizi wa huduma (kadi 9 ): zikionesha shughuli muhimu ambazo
watu wanaweza kufanya kupambana na matatizo ambayo huwakumba akinamama na
watoto wachanga pale yanapoibuka
Mkutano wa 3:
Kubaini matatizo yanayowakumba watoto wachanga chini ya wiki 4
Malengo
ya mkutano ni kubaini matatizo yanayowakumba watoto wakati wa ujauzito, wakati
wa kujifungua na baada ya kujifungua; kujadili hali
halisi ya matunzo ya watoto wachanga chini ya wiki 4 nyumbani; na kujadili kwa
nini, lini na jinsi gani wanawake
hutafuta msaada.
Mkutano wa 4: Kuweka vipaumbele
Lengo la
mkutano huu ni kubaini matatizo makubwa 3 kwa
afya ya akinamama na watoto wachanga ambayo yatapewa kipaumbele katika mzunguko
huu.
Mkutano wa 5: Kubaini mambo yanayochangia
Lengo la
mkutano ni kubaini visababishi vya matatizo makubwa ambayo yameamuliwa kupewa
kipaumbele
MZUNGUKO WA UTENDAJI
WA KIKUNDI CHA TUSHIKAMANE
Awamu ya
2: Kubaini pamoja ufumbuzi.
Shabaha
ya Awamu ya 2 ya mzunguko wa mikutano ya Kikundi ni kupanga ufumbuzi wa matatizo yanayowakumba
akinamama na watoto wachanga
Mkutano wa 6: Kubaini shughuli za uzuiaji na
usimamizi wa matatizo
Malengo ya
mkutano ni:
·
Kubaini
shughuli ambazo zinaweza kuzuia matatizo makubwa yanayowakumba akinamama na
watoto kutokea.
·
Kubaini
shughuli kwa ajili ya usimamizi wa
matatizo makubwa ya afya ya akinamama na watoto wachanga chini ya wiki 4 kama
tayari yapo
Mkutano wa 7: Kubaini ufumbuzi
Malengo ya mkutano ni:
·
Kubaini njia za ufumbuzi kwa ajili ya kuzuia na
kusimamia matatizo yaliyopewa kipaumbele.
·
Kubaini rasilimali au nyenzo ambazo zinaweza
kusaidia na vikwazo ambavyo vinaweza kuzuia utekelezaji wa njia za ufumbuzi. (mathalan
makundi yote 2-wafanyakazi wa afya vijijini na wakunga wasaidizi wanaweza
kusaidia kufanikisha masuala mbalimbali kama vile unyonyeshaji,uzazi wa mpango;
chanjo; usafi; uzuiaji malaria; na utambuzi wa dalili za ugonjwa kali.)
Kutokana na uzoefu, njia nyingi za kawaida za ufumbuzi wa matatizo zinazobainishwa na
vikundi ni pamoja na:
·
Elimu
ya afya
·
Usafiri
·
Mfuko
wa kikundi wa akiba
·
Vifaa safi kwa ajili
ya kujifungua
·
Shughuli
za kuongeza pato
·
Mafunzo
kwa wakunga wa jadi
·
Kushirikiana
na ushawishi kwa vituo vya kutolea huduma za afya
·
Bustani
za mbogamboga
Baada ya
Mkutano wa 7, wanakikundi wanapaswa kukutana kwa ajili ya kuandaa na kufanya
mazoezi ya mrejesho kwa jamii katika kikao kinachofuata.
Mkutano wa 8: Kutoa mrejesho juu
ya maendeleo ya mikutano kwa jamii
Malengo
ya mkutano ni :
·
Kutoa
mrejesho kutokana na mijadala kwa
wanajamii wote, ikijumuisha matatizo ambayo imeamuliwa yapewe kipaumbele na
ufumbuzi wake.
·
Kukusanya
mawazo na maoni ya wanajamii wote juu ya masuala mbalimbali yaliyojadiliwa
na kikundi.
·
Kupata
msaada wa hali na mali kutoka kwa
wanajamii wote kwa ajili ya utekelezaji wa njia za ufumbuzi zilizobainishwa.
MZUNGUKO WA
UTENDAJI WA KIKUNDI CHA TUSHIKAMANE
Awamu ya 3:
Kutekeleza kwa pamoja njia za ufumbuzi
Shabaha
ya Awamu ya 3 ya mzunguko wa mikutano ni Kikundi kiweze kutekeleza njia za
ufumbuzi zilizobainishwa ili kukabiliana na matatizo ya afya ya akinamama na
watoto wachanga.
Mkutano wa 9: Kupanga njia za ufumbuzi
Malengo ya mkutano ni:
·
Kupata ushirikiano na maelewano kutoka kwa wadau
wote kuhusiana na njia za ufumbuzi zilizopendekezwa
·
Kukamilisha na kuuafiki mpangokazi kwa ajili ya njia za ufumbuzi .
Mkutano wa 10: Kukusanya rasilimali
Lengo la mkutano ni kupanga jinsi ya kukusanya rasilimali
ambazo zinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa njia za ufumbuzi.
Ukusanyaji rasilimali
Baada ya Mkutano wa 10 wanakikundi wanapaswa kuanza utafutaji na ukusanyaji wa rasilimali
mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za ufumbuzi.
Mkutano wa 11: Kuandaa
zana za ufuatiliaji
Lengo la
mkutano ni kupanga jinsi ya kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa shughuli za
ufumbuzi.
Utekelezaji na
ufuatiliaji wa shughuli za ufumbuzi
Baada ya
Mkutano wa 11, wanakikundi wanapaswa
kutekeleza na kufuatilia shughuli zao za ufumbuzi. Wanatakiwa kuifanya kazi hii kwa kipindi cha miezi 3 hadi 6. Vikundi
na vikosikazi wakutane mara kwa mara na
mwezeshaji wao katika kipindi hiki, kupitia maendeleo ya utekelezaji, kusherekea
mafanikio na kubaini na kuzifanyia kazi changamoto zozote. Ratiba ya kufanyika
kwa mikutano itaamuliwa na wanakikundi wenyewe.
MZUNGUKO WA UTENDAJI WA KIKUNDI CHA TUSHIKAMANE
Awamu 4: Kutathmini pamoja
Shabaha ya Awamu ya
4 ya mzunguko wa mikutano na kutathmini matokeo ya shughuli za ufumbuzi
ambazo zimetekelezwa juu ya matatizo ya akinamama na watoto wachanga
yaliyobainishwa.
Mkutano
wa 12: Kuandaa kutathmini
Malengo
ya mkutano ni:
·
Kuchunguza kwa nini kutathmini pamoja
kikundi na shughuli za ufumbuzi ni muhimu.
·
Kujiandaa na kupanga kwa ajili ya zoezi la tathmini
Kukusanya
data kwa ajili ya tathmini
Baada
ya Mkutano wa 12, wanakikundi wanapaswa
kwa pamoja kukusanya data wanazohitaji kwa ajili ya tathmini.
Mkutano
wa 13: Kutathmini matokeo ya shughuli za
ufumbuzi juu ya matatizo yaliyopewa kipaumbele
Malengo ya mkutano ni:
·
Kutathmini kwa kiwango gani cha ufanisi matatizo
yaliyopewa kipaumbele yameshughulikiwa
·
Kutathmini utendaji wa Kikundi
·
Kupanga kwa ajili ya wakati ujao.
Mkutano wa 14: Kupanga kwa ajili ya wakati
ujao
Lengo
la mkutano ni kuamua Kikundi kifanye nini baada ya hapo.
Anza
upya mzunguko wa utendaji
Baada
ya Mkutano wa 14, Kikundi kinapaswa
kuwezeshwa kuanzisha tena mzunguko
katika Awamu ya 1, 2 au 3 kutegemea na kipi kilijadiliwa na kuamuliwa
katika mkutano.
Baada
ya mzunguko 1 wa mikutano ya kikundi, Kikundi kinapaswa kujisikia kuwa
kinaimiliki programu na kuwa na uwezo wa
kuendelea kukutana. Wajibu wa wasimamizi na viongozi ni kuwepo kwa ajili ya
kuendelea kutoa ushauri wa kitaalam, lakini dira na shabaha ya kikundi viamuliwe
na wanakikundi wenyewe.
No comments:
Post a Comment